Oktoba 7, 2024,
Na Job Karongo, Handeni-TC
Halmashauri ya Mji Handeni imezindua mafunzo maalum ya usimamizi na utoaji wa mikopo kwa Kamati za Usimamizi wa Mikopo za Kata. Mafunzo haya yamehusisha kamati kutoka kata zote 12 zinazounda Halmashauri ya Mji Handeni, yakilenga kuimarisha uwezo wa kamati hizo katika kusimamia utoaji wa mikopo kwa ufanisi na uadilifu.
Mada kuu iliyojadiliwa katika mafunzo hayo ilikuwa ni muongozo na kanuni za usimamizi wa mikopo kwa makundi maalum, yakiwemo Wanawake, Vijana, na Watu wenye Ulemavu. Mafunzo haya yanalenga kuhakikisha makundi haya yanafaidika ipasavyo na mikopo inayotolewa kwa asilimia 10, kama inavyoelekezwa na Serikali.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji handeni, Bw. Gerald Kauki, amesisitiza umuhimu wa uadilifu na uwajibikaji katika usimamizi wa mikopo hiyo. Ameeleza kuwa mafanikio ya mpango huu yanategemea utawala bora, na akaongeza kuwa jukumu kubwa la kamati ni kuhakikisha rasilimali za mikopo zinasimamiwa kwa weledi ili kuwafikia walengwa waliokusudiwa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Divisheni ya Maendeleo ya Jamii, Bwana Fredy Mpondachuma, amesisitiza kuwa kamati hizi zinapaswa kufanya kazi kwa ufanisi ili kufikia matarajio ya Serikali na wananchi. Aidha, ameahidi kuzisimamia kwa ukaribu kamati hizo ili kuhakikisha zinafuata maelekezo na taratibu zilizowekwa.
Wajumbe wa kamati walioshiriki mafunzo wameonyesha nia ya dhati ya kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi, wakiahidi kuhudumia wananchi kwa umakini na kuwafikia walengwa kwa usawa. Pia, Kaimu Mkurugenzi ameweka wazi kuwa ni muhimu kuhakikisha kwamba walengwa wote, hata wale walioko mbali na makao makuu ya kata, wanapata fursa ya kupewa mikopo bila upendeleo.
Mafunzo haya yanatoa mwongozo thabiti katika kusimamia rasilimali za mikopo kwa makundi maalum na yanaweka msingi wa kuongeza ufanisi katika utoaji wa mikopo kwa walengwa wenye mahitaji.
Barabara ya Korogwe - Handeni
Anuani ya Posta: S.L.P 51 HANDENI
Simu ya Mezani: 027-2641807
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: td@handenitc.go.tz
Copyright ©2022 GWF . All rights reserved.